UJUMBE WA MWENYEKITI WA ISLAMIC CENTRE FOR RESEARCH (ICR) SIKU YA UZINDUZI WA PROGRAMU ZA ICR, TAREHE 23/2/2012

24 Feb

Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu. Rehma na amani za milele zimfikie kipenzi cha Mwenyezi Mungu, Mtume wa amani, Nuru ya ulimwengu, Mtume wa rehma, Mtume Mteule, Muhammad al-Mustafa (s.a.w).

Pia rehma na amani ziwe juu ya ahli zake, Maswahaba na wale wote wenye kufuata mwenendo wao mwema mpaka siku ya malipo.

Ndugu zangu katika imani,

Assalaam alaykum warahmatullah wabarakaatuh!

Ninachukua nafasi hii kuwashukuru masheikh wetu pamoja na waumini wote kwa kuacha shughuli zenu na kuja kuungana nasi katika kuadhimisha mazazi ya Mtume wetu (s.a.w), ambaye alitumwa kuwa rehma kwa walimwengu wote, yaani wanadamu na viumbe vingine vyote.

Maadhimisho haya yameandaliwa na Kituo cha Utafiti cha Kiislamu (yaani Islamic Centre for Research –ICR).

ICR NI NINI?

MAELEZO MAFUPI KUHUSU ICR

ISLAMIC CENTRE FOR RESEARACH ni taasisi ya Kiislamu iliyoanzishwa kwa ajili ya kuhamasisha maarifa ya kuuelewa Uislamu na mafundisho yake matukufu kwa wanadamu kwa kutumia hekma, busara na mawaidha mazuri kama asemavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.” (Qur’an 16: 125)

Aya ifuatayo ilitupa msukumo mwingine wa kuanzisha kituo hiki muhimu kwa Waislamu:

“Sema: Hii ndiyo Njia yangu – ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua – mimi na wanao nifuata.” (Qur’an 12: 108) kwa sababu inatutaka sisi Waislamu –ambao ni Wafuasi wa Mtume (s.a.w) – kuijua dini yetu kwa undani kabisa.

MALENGO NA MADHUMUNI YA ICR

Kutoka na  kuusoma ujumbe huo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu nilioueleza hapo juu, tulihamasika kuanzisha kituo hiki kikiwa na malengo kadhaa wa kadhaa ya kiroho. Miongoni mwa malengo hayo ni pamoja na:

 1. Kuandika, kutafsiri na kuchapisha vitabu mbalimbali vya Kiislamu kutoka katika lugha za kigeni kuja katika lugha yetu ya Kiswahili. Tumeweka mkazo mkubwa sana katika kutafsiri vitabu kutokana na ukweli kwamba, vitabu vingi vya maarifa ya dini yetu tukufu vipo katika lugha za kigeni kama vile: Kiarabu, Kiingereza, Kituruki n.k, na Waislamu walio wengi hawazifahamu lugha hizi kwa kiwango cha kutosha kuielewa dini yao. Hivyo tukaamua kujitolea kufanya kazi hii na kulibeba jukumu hili muhimu sana.

 

 1. Kuhamasisha amani, heshima, upendo  na huruma baina ya watu wote ili wapate kuitambua tunu ya udugu wa kibinaadamu ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia. Tukiwa na mambo hayo tutakuwa na jamii bora, imara na yenye ustawi na maendeleo.

 

 1. Kutoa huduma za kibinaadamu kama vile elimu, afya na misaada maalumu kupitia shughuli mbalimbali za kimisaada bila kuumiza heshima na utu wa wahusika.

 

Hayo ni baadhi tu miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa Kituo cha Utafiti cha Kiislamu.

 

PROGARMU NA HARAKATI MBALIMBALI ZA ICR

Ndugu Waislamu,

Katika kutimiza malengo mbalimbali ya kuanzishwa kwake, ICR imekuwa ikiendesha programu kadhaa wa kadhaa. Miongoni mwa programu hizo ni pamoja na:

 1. KIPINDI CHA REDIO: Kipindi hiki hurushwa kila wiki katika siku za Jumanne, kuanzia saa 3:00 usiku kupitia idhaa ya Redio Sauti ya Qur’an ya jijini Dar es Salaam. Katika kipindi hiki, maofisa wa ICR wakiongozwa na Katibu Mkuu ndugu Ibrahimu Hamisi Kabuga huwasilisha mada mbalimbali zinazohusu dini yetu tukufu na kutoa elimu kwa umma wa Kiislamu na Tanzania kwa ujumla. Kipindi hiki husikika katika mikoa mitano ya Tanzania bara na visiwani. Kwa Dar es Salaam, kipindi hiki husikika kupitia masafa ya 102 FM.

Aidha, kipindi hiki hakina mfadhili rasmi, bali huendeshwa kwa michango ya wana – ICR wenyewe.

 

 1. PROGRAMU YA KUTAFSIRI VITABU: Kama nilivyosema hapo awali, miongoni mwa malengo ya ICR ni kutafsiri vitabu mbalimbali vya dini yetu kutoka katika lugha za kigeni kuja katika Kiswahili. Tangu kuanza kwa mpango huu vitabu vipatavyo 34 vimetafsiriwa kutoka katika lugha za Kiingereza na Kiarabu kuja katika Kiswahili. Hata hivyo, kutokana na uchanga wa taasisi yetu hii, ni vitabu 8 tu ndivyo vilivyochapishwa mpaka sasa. Vitabu vinavyochapishwa hutolewa bure kwa Waislamu na wale wanaotaka kuijua dini yetu tukufu.

Miongoni mwa vitabu vilivyotafsiriwa ni pamoja na:

 

–          Islam on Trial (Uislamu Mahakamani)

–           The Qur’an is Amazing (Qur’an ni ya ajabu)

–          The examplary beyond compare, Muhammad Mustafa (Kiigizo kisichokuwa na mfano, Muhammad Mustafa (s.a.w)

–          The Last Breath (pumzi ya mwisho)

–          Islam: Spirit and Form (Uislamu: Imani na Matendo)

– Endowment, charity and services in Islam (Wakfu, Sadaka na Huduma katika Uislamu)

– The story of the reed (simulizi ya filimbi ya mwanzi)

–          Na vingine vingi

 

Ni matarajio yetu kuwa kadiri tutakavyozidi kupata uwezo tutazidi kutafsiri na kuchapisha vitabu vingine.

 

 1. PROGARMU YA ELIMU MASHULENI: Katika programu hii maofisa wa ICR wamekuwa wakitembelea shule mbalimbali za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam na kutoa elimu ya kiroho, kujibu maswali yanayoulizwa na vijana na kugawa makala na vitabu vinavyoandaliwa na ICR. Tunataraji kuendelea na mpango huu inshaallah.

 

 1. PROGRAMU YA MAARIFA VIJIJINI: ICR imekuwa ikifanya programu za vijijini pia. Mwaka jana ICR ilifanya ziara katika vijiji 10 vya mikoa ya Tabora, Shinyanga na Kigoma kwa ajili ya kutoa maarifa ya dini kwa vijana na wanawake wa vijiji hivyo. Tunataraji kuwa programu hii itaendelea mwaka huu kwa kuongeza wigo wa vijiji vitakavyotembelewa.

 

 1. MAKONGAMANO: Tumekuwa tukifanya makongamano kwa ajili ya kuelimisha umma wetu kuhusu dini yetu Tukufu ya Kiislamu na mafundisho yake adhimu. Miongoni mwa makongamano hayo ni Kongamano la wanawake wa Kiislamu lililofanyika katika ukumbi wa Markaz Chang’ombe, na lile la “Mtume Muhammad (s.a.w) na Vijana” lililofanyika katika ukumbi wa Al-haramain, Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambalo lilihudhuriwa na ndugu zetu kutoka Uturuki na Azerbaijan.

 

 1. DAAWAH KATIKA INTERNET: Ndugu zangu Waislamu, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) imekuwa ni chombo muhimu cha kuwaunganisha watu ulimwenguni. Kwa sasa imekuwa rahisi kwa mtu wa bara la Afrika kuwasiliana na mtu wa bara la Asia na mabara mengine kwa njia nyepesi na bila gharama kubwa. Kwa kutambua nguvu ya mawasiliano ya ki-elektroni, ICR ilitengeneza blog katika mtandao ambao unatoa elimu na kuonyesha harakati mbalimbali za ICR. Blog hiyo ni: http://www.icrtz.wordpress.com

 

Mbali na blog hiyo, pia kuna ukumbi maalumu katika mtandao wa kijamii wa facebook wenye jina la ISLAMIC CENTRE FOR RESEARCH (ICR). Ukumbi huu una wanachama wapatao 2800 kutoka nchi mbalimbali duniani. Kupitia ukumbi huu, watu huweza kupata maarifa na vitabu mbalimbali kutoka ICR. Tunajitahidi kuendelea kuboresha huduma zetu kwa njia ya ki-elektroniki kadiri uwezo utakavyoruhusu inshaallah.

 

Ndugu zangu Waislamu, ICR ina programu nyingi ambazo zinatekelezwa kwa sasa na baadhi zinatarajiwa kuanza kutekelezwa muda si mrefu na muda huo ukifika tutazitangaza.

 

Kwa hakika ni mengi ya kuzungumza, lakini la msingi ni kuwa ICR bado ina nafasi kubwa ya kusonga mbele iwapo itapata ushirikiano kutoka kwenu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema kuwa: “Saidianeni katika wema na uchamungu”. Hivyo tukisaidiana tutaweza kutimiza malengo ya kuumbwa kwetu.

 

Naomba nichukua fursa hii kuwatakia sherehe njema ya mazazi ya Mtume (s.a.w) na uzinduzi wa programu za ICR kwa mwaka huu wa 2012.

 

Allah atufanyie wepesi, sisi na nyinyi pia.

 

Wassalaam alaykum warahmatullah

Advertisements

2 Responses to “UJUMBE WA MWENYEKITI WA ISLAMIC CENTRE FOR RESEARCH (ICR) SIKU YA UZINDUZI WA PROGRAMU ZA ICR, TAREHE 23/2/2012”

 1. Ally Bakari Mbwambo March 15, 2012 at 3:11 pm #

  Kwa mara ya kwanza kujiunga na web yenu nimefarijika sana,hongereni hakuna awezaye kuwalipa harakati zenu zaidi ya allah, hasa kama munafanya kazi kwa ajili yake.

 2. Mohamed Abdirahman Aidarus March 16, 2012 at 2:46 pm #

  A.aleykum wr,wb.MashaAllah.Nimefurahi sana kuona harakati kama hizi zinafanyika.Wallah hamjui tu furaha niliokuwa nayo sasa hivi.Allah afungue njia zote za khair ili tuweze kusimama kidete kutetea haki za waislamu.Ni jukumu la kila mmoja wetu kuhamasisha walio kata tamaa,walio kaa kimya na kuelimisha jamii kwa kutoa taarifa mbali mbali.
  In Sha Allah tuweze kukutana siku moja kati ya viongozi na stakeholders tuweze kutoa maoni yetu.

  Baarakallahu fikum.

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s

%d bloggers like this: