TANGAZO LA MASHINDANO YA KIMATAIFA

12 Mar

Al Azhar Al Sharif

Mkusaanyiko wa Tafitit za Kiislamu

Idara kuu ya Mambo ya Baraza la Mkusanyiko na Kamati zake.

(Uwezo wa Kuran Tukufu na Sunnah za Mtume S.A.W. zilizotakasika juu ya mwenendo wa Elimu ya Mazingira)

 Kamati ya Uwezo wa elimu ya Kuran na Sunnah za Mtume Mtakasifu ya Azhar Asharif kwa kushirikiana na Bank Faisal ya Kiislamu tawi la Egypt, inawatangazia kuwa itaandaa Mashindano ya Kimataifa juu ya “Uwezo wa Kuran Tukufu na Sunnah za Mtume S.A.W zilizotakasika juu ya mwenendo wa Elimu ya Mazingira) kwa masharti yafuatayo:-

Mosi: – Utafiti uandikwe kati ya lugha mbili: – Kiarabu au Kiingereza.

Pili: – Utafiti utakaoletwa kwa mshindano usiwe kwa kiwango cha kielimu au umepewa zawadi nyingine.

Tatu: – Utafiti uweke wazi juu ya uhakika wa kielimu ambao umetanguliwa na Kuran pamoja na Sunnah Takasifu.

Nne: – Utafiti uandikwe kwa Kompyuta na usipungue kurasa mia moja na zisizidi kurasa mia mbili, pamoja na Ufupisho ulio nje ya Utafiti usiopungua kurasa kumi na usiozidi kurasa ishirini pamoja na CD inayohusu utafiti huo.

Tano:- Utafiti pamoja na Ufupisho wake upelekwe na taarifa binafsi ya mashirika (C.V.) kwa nakala tatu kwenye Kamati ya Uwezo wa Kuran Tukufu na Sunnah za Mtume – Mkusanyiko wa Tafiti za Kiislamu Nasr City mpaka mwisho wa mwezi Mei 2012 na mpelekaji wa utafiti huo atapewa risiti iliyogongwa.

Sita: – Baada ya kupitiwa kwa tafiti na wahusika washindanaji wataitwa wenyewe kwa wale waliopendekezwa kufuzu na kupewa zawadi za mali kwa kiwango cha:-  Paundi Elfu Hamsini na Tano za Kimisri (55,000/=) kwa washindani ishirini na tatu (23) kama ifuatavyo:-  Paundi 15,000 elfu kumi na tano kwa mshindi wa kwanza.  Paundi 10,000 elfu kumi kwa mshindi wa pili.  Paundi 5,000 elfu tano kwa ,mshindi wa tatu.

Na zawadi tano (5) za kutia moyo zitatolewa kwa watu watano ikiwa kila mmoja atapata Paundi Elfu mbili (2,000/=)

Na zawadi kumi na tano (15) nyingine za kutia moyo zitatolewa kwa watu watano ikiwa kila mmoja atapata Paundi Elfu moja (1,000/=)

Saba: – Watapewa taarifa washiriki wa shindano sehemu na siku ya sherehe ya kuzawadia washindi.

Nane: – Tafiti iliyoshinda haitarejeshwa kwa mwenyewe, kwani tafiti hiyo itahifadhiwa kwenye ofisi za Kamati maalum kwenye jingo la ofisi za Azhar Asharif, ama kwa tafiti zisizoshinda zitarudishwa kwa wenyewe kwa kipindi cha miezi miwili tokea tarehe ya sherehe ya kugawa zawadi.

Tisa: – Kwa mwenye kutaka kujifanyia waqfu achapishe na kusambaza yale atakayopata toka kwemye tafiti ya mshindi, kwa gharama ya waqfu bila idhini na haki toka kwa mshindi.

Kumi:-Tangazo hili linahusu Vyuo vVkuu vyote na Vituo vya eEimu pamoja na Magazeti na wasambazaji – kama habari isiyo na malipo – kwa Magazeti na Majarida mbalimbali.

Mwenyezi Mungu ndiye Mwezeshaji wa kila jambo.

Kamati ya uwezo wa Elimu ya Kuran Tukufu na Sunnah za Mtume zilizotakaswa Mkusanyiko wa Tafiti za Kiislamu

Advertisements

UGONJWA WA KICHOCHO (BILHARZIA)

11 Mar
Tatizo hili huwapata watu wengi hasa watoto wanaocheza katika madimbwi ya maji wakati wa mvua au wanapotumia maji ambayo yana vijidudu vya maradhi hayo. Vijidudu vya kichocho humuingia binadamu na kwenda kuishi katika kibofu cha mkojo au utumbo wake.
Kwa kawaida kimelea cha kike hutaga mayai ambayo hutoka kwa mtu mwenye ugonjwa huo na kuingia katika maji ikiwa mtu huyo atakojolea maji hayo au wakati wa haja kubwa. Mayai hayo huanguliwa na kutoa viluilui ambavyo hupenya kwa konokono wa majini. Viluilui hawa baada kutoka kwenye mwili wa konokono huweza kumuingia binadamu na kupenya katika ngozi na kwenda kutulia ktka mishipa ya ini ambapo hukomaa na baada ya hapo hutoka na kuingia katika mishipa ya kibofu cha mkojo na njia ya haja kubwa  katika utumbo mpana.
Mgonjwa asipotibiwa haraka hupata matatizo katika njia ya haja kubwa na kibofu cha mkojo na wakati mwingine mayai ya kichocho huingia katika uti wa mgongo au katika ubongo na kusababisha matatizo.
DALILI
Kupatwa na homa siku 30 baada ya kunywa maji yenye maambukizi
Kikohozi kikavu na kujihisi kuchoka.
Baadaye damu huanza kutoka kwenye mkojo na haja kubwa lakini hatua hii ni baada ya ugonjwa kukomaa.
USHAURI
Kichocho ni ugonjwa unaotibika haraka kwa dawa iwapo itabainika mapema.
Watoto wazuiwe kuogelea katika madimbwi au maji yaliyosimama.
Kunywa maji masafi na salama.
Wanaoish kando ya mito, maziwa na bahari wasikanyage maji hayo bila kuwa na viatu maalumu vya kuzuia maji kupenya na mabwawa yote ya kuogelea yawekwe dawa ya kuua vijidudu.
MAKALA HAYA YAMEANDALIWA NA DOKTA ABDULAZIZI MALIKI (+255 714 909 563/ +255 763 986 499)

UJUMBE WA MWENYEKITI WA ISLAMIC CENTRE FOR RESEARCH (ICR) SIKU YA UZINDUZI WA PROGRAMU ZA ICR, TAREHE 23/2/2012

24 Feb

Kila sifa njema anastahiki Mwenyezi Mungu, Mwingi wa rehma, Mwenye kurehemu. Rehma na amani za milele zimfikie kipenzi cha Mwenyezi Mungu, Mtume wa amani, Nuru ya ulimwengu, Mtume wa rehma, Mtume Mteule, Muhammad al-Mustafa (s.a.w).

Pia rehma na amani ziwe juu ya ahli zake, Maswahaba na wale wote wenye kufuata mwenendo wao mwema mpaka siku ya malipo.

Ndugu zangu katika imani,

Assalaam alaykum warahmatullah wabarakaatuh!

Ninachukua nafasi hii kuwashukuru masheikh wetu pamoja na waumini wote kwa kuacha shughuli zenu na kuja kuungana nasi katika kuadhimisha mazazi ya Mtume wetu (s.a.w), ambaye alitumwa kuwa rehma kwa walimwengu wote, yaani wanadamu na viumbe vingine vyote.

Maadhimisho haya yameandaliwa na Kituo cha Utafiti cha Kiislamu (yaani Islamic Centre for Research –ICR).

ICR NI NINI?

MAELEZO MAFUPI KUHUSU ICR

ISLAMIC CENTRE FOR RESEARACH ni taasisi ya Kiislamu iliyoanzishwa kwa ajili ya kuhamasisha maarifa ya kuuelewa Uislamu na mafundisho yake matukufu kwa wanadamu kwa kutumia hekma, busara na mawaidha mazuri kama asemavyo Mwenyezi Mungu Mtukufu:

“Waite waelekee kwenye Njia ya Mola wako Mlezi kwa hikima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora. Hakika Mola wako Mlezi ndiye anaye mjua zaidi aliye ipotea Njia yake, na Yeye ndiye anaye wajua zaidi walio ongoka.” (Qur’an 16: 125)

Aya ifuatayo ilitupa msukumo mwingine wa kuanzisha kituo hiki muhimu kwa Waislamu:

“Sema: Hii ndiyo Njia yangu – ninalingania kwa Mwenyezi Mungu kwa kujua – mimi na wanao nifuata.” (Qur’an 12: 108) kwa sababu inatutaka sisi Waislamu –ambao ni Wafuasi wa Mtume (s.a.w) – kuijua dini yetu kwa undani kabisa.

MALENGO NA MADHUMUNI YA ICR

Kutoka na  kuusoma ujumbe huo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu nilioueleza hapo juu, tulihamasika kuanzisha kituo hiki kikiwa na malengo kadhaa wa kadhaa ya kiroho. Miongoni mwa malengo hayo ni pamoja na:

 1. Kuandika, kutafsiri na kuchapisha vitabu mbalimbali vya Kiislamu kutoka katika lugha za kigeni kuja katika lugha yetu ya Kiswahili. Tumeweka mkazo mkubwa sana katika kutafsiri vitabu kutokana na ukweli kwamba, vitabu vingi vya maarifa ya dini yetu tukufu vipo katika lugha za kigeni kama vile: Kiarabu, Kiingereza, Kituruki n.k, na Waislamu walio wengi hawazifahamu lugha hizi kwa kiwango cha kutosha kuielewa dini yao. Hivyo tukaamua kujitolea kufanya kazi hii na kulibeba jukumu hili muhimu sana.

 

 1. Kuhamasisha amani, heshima, upendo  na huruma baina ya watu wote ili wapate kuitambua tunu ya udugu wa kibinaadamu ambao Mwenyezi Mungu amewajaalia. Tukiwa na mambo hayo tutakuwa na jamii bora, imara na yenye ustawi na maendeleo.

 

 1. Kutoa huduma za kibinaadamu kama vile elimu, afya na misaada maalumu kupitia shughuli mbalimbali za kimisaada bila kuumiza heshima na utu wa wahusika.

 

Hayo ni baadhi tu miongoni mwa malengo ya kuanzishwa kwa Kituo cha Utafiti cha Kiislamu.

 

PROGARMU NA HARAKATI MBALIMBALI ZA ICR

Ndugu Waislamu,

Katika kutimiza malengo mbalimbali ya kuanzishwa kwake, ICR imekuwa ikiendesha programu kadhaa wa kadhaa. Miongoni mwa programu hizo ni pamoja na:

 1. KIPINDI CHA REDIO: Kipindi hiki hurushwa kila wiki katika siku za Jumanne, kuanzia saa 3:00 usiku kupitia idhaa ya Redio Sauti ya Qur’an ya jijini Dar es Salaam. Katika kipindi hiki, maofisa wa ICR wakiongozwa na Katibu Mkuu ndugu Ibrahimu Hamisi Kabuga huwasilisha mada mbalimbali zinazohusu dini yetu tukufu na kutoa elimu kwa umma wa Kiislamu na Tanzania kwa ujumla. Kipindi hiki husikika katika mikoa mitano ya Tanzania bara na visiwani. Kwa Dar es Salaam, kipindi hiki husikika kupitia masafa ya 102 FM.

Aidha, kipindi hiki hakina mfadhili rasmi, bali huendeshwa kwa michango ya wana – ICR wenyewe.

 

 1. PROGRAMU YA KUTAFSIRI VITABU: Kama nilivyosema hapo awali, miongoni mwa malengo ya ICR ni kutafsiri vitabu mbalimbali vya dini yetu kutoka katika lugha za kigeni kuja katika Kiswahili. Tangu kuanza kwa mpango huu vitabu vipatavyo 34 vimetafsiriwa kutoka katika lugha za Kiingereza na Kiarabu kuja katika Kiswahili. Hata hivyo, kutokana na uchanga wa taasisi yetu hii, ni vitabu 8 tu ndivyo vilivyochapishwa mpaka sasa. Vitabu vinavyochapishwa hutolewa bure kwa Waislamu na wale wanaotaka kuijua dini yetu tukufu.

Miongoni mwa vitabu vilivyotafsiriwa ni pamoja na:

 

–          Islam on Trial (Uislamu Mahakamani)

–           The Qur’an is Amazing (Qur’an ni ya ajabu)

–          The examplary beyond compare, Muhammad Mustafa (Kiigizo kisichokuwa na mfano, Muhammad Mustafa (s.a.w)

–          The Last Breath (pumzi ya mwisho)

–          Islam: Spirit and Form (Uislamu: Imani na Matendo)

– Endowment, charity and services in Islam (Wakfu, Sadaka na Huduma katika Uislamu)

– The story of the reed (simulizi ya filimbi ya mwanzi)

–          Na vingine vingi

 

Ni matarajio yetu kuwa kadiri tutakavyozidi kupata uwezo tutazidi kutafsiri na kuchapisha vitabu vingine.

 

 1. PROGARMU YA ELIMU MASHULENI: Katika programu hii maofisa wa ICR wamekuwa wakitembelea shule mbalimbali za sekondari za mkoa wa Dar es Salaam na kutoa elimu ya kiroho, kujibu maswali yanayoulizwa na vijana na kugawa makala na vitabu vinavyoandaliwa na ICR. Tunataraji kuendelea na mpango huu inshaallah.

 

 1. PROGRAMU YA MAARIFA VIJIJINI: ICR imekuwa ikifanya programu za vijijini pia. Mwaka jana ICR ilifanya ziara katika vijiji 10 vya mikoa ya Tabora, Shinyanga na Kigoma kwa ajili ya kutoa maarifa ya dini kwa vijana na wanawake wa vijiji hivyo. Tunataraji kuwa programu hii itaendelea mwaka huu kwa kuongeza wigo wa vijiji vitakavyotembelewa.

 

 1. MAKONGAMANO: Tumekuwa tukifanya makongamano kwa ajili ya kuelimisha umma wetu kuhusu dini yetu Tukufu ya Kiislamu na mafundisho yake adhimu. Miongoni mwa makongamano hayo ni Kongamano la wanawake wa Kiislamu lililofanyika katika ukumbi wa Markaz Chang’ombe, na lile la “Mtume Muhammad (s.a.w) na Vijana” lililofanyika katika ukumbi wa Al-haramain, Kariakoo jijini Dar es Salaam, ambalo lilihudhuriwa na ndugu zetu kutoka Uturuki na Azerbaijan.

 

 1. DAAWAH KATIKA INTERNET: Ndugu zangu Waislamu, teknolojia ya habari na mawasiliano (ICT) imekuwa ni chombo muhimu cha kuwaunganisha watu ulimwenguni. Kwa sasa imekuwa rahisi kwa mtu wa bara la Afrika kuwasiliana na mtu wa bara la Asia na mabara mengine kwa njia nyepesi na bila gharama kubwa. Kwa kutambua nguvu ya mawasiliano ya ki-elektroni, ICR ilitengeneza blog katika mtandao ambao unatoa elimu na kuonyesha harakati mbalimbali za ICR. Blog hiyo ni: http://www.icrtz.wordpress.com

 

Mbali na blog hiyo, pia kuna ukumbi maalumu katika mtandao wa kijamii wa facebook wenye jina la ISLAMIC CENTRE FOR RESEARCH (ICR). Ukumbi huu una wanachama wapatao 2800 kutoka nchi mbalimbali duniani. Kupitia ukumbi huu, watu huweza kupata maarifa na vitabu mbalimbali kutoka ICR. Tunajitahidi kuendelea kuboresha huduma zetu kwa njia ya ki-elektroniki kadiri uwezo utakavyoruhusu inshaallah.

 

Ndugu zangu Waislamu, ICR ina programu nyingi ambazo zinatekelezwa kwa sasa na baadhi zinatarajiwa kuanza kutekelezwa muda si mrefu na muda huo ukifika tutazitangaza.

 

Kwa hakika ni mengi ya kuzungumza, lakini la msingi ni kuwa ICR bado ina nafasi kubwa ya kusonga mbele iwapo itapata ushirikiano kutoka kwenu. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema kuwa: “Saidianeni katika wema na uchamungu”. Hivyo tukisaidiana tutaweza kutimiza malengo ya kuumbwa kwetu.

 

Naomba nichukua fursa hii kuwatakia sherehe njema ya mazazi ya Mtume (s.a.w) na uzinduzi wa programu za ICR kwa mwaka huu wa 2012.

 

Allah atufanyie wepesi, sisi na nyinyi pia.

 

Wassalaam alaykum warahmatullah

MUUJIZA WA MBU -1

13 Feb

Kazi nyingi zinazofanywa na wanyama na matendo yao vinahitaji kiwango cha utambuzi, uzoefu, maarifa na utaalamu unaokwenda mbali zaidi ya kile wanachokifanya kwa kutumia kiwango cha akili walichonacho. Uchunguzi mdogo tu unatutosha kabisa kujua kwamba sio wanyama kama wao wanaotoa sifa hizo bora.

Fikiria uwezo wa ndege wanaohama maelfu ya kilomita wakiwa angani bila kuchoka,  usanifu wenye ujuzi wa ajabu unaotumiwa na buibui wakati kutengeneza mtandao wa nyuzi zake,  ushirikiano kamili na ugawanaji wa majukumu katika makoloni na himaya za wadudu chungu, jiometri ya ajabu ya katika masega ya asali yaliyojengwa kwa ushirikiano na maelfu ya nyuki, na mifano mingine mingi isiyohisabika…

Chanzo cha akili na utashi huu unaowawezesha wanyama ya kufanya mambo haya hakipatikani ndani ya  miili yao wala katika maumbile yao, bali kinapatikana katika uingiliaji kati wa ajabu wa akili na nguvu isiyoonekana ambayo hujidhihirisha katika kila hatua. Hata kama mmiliki wa akili na nguvu hii haonekani, uingiliaji kati huu katika matukio mbalimbali hutoa ushahidi wa kutosha wa kuwepo kwa nguvu hii ili kuondoa mashaka yote.

Wanasayansi wenye kufuata nadharia ya mgeuko (evolitionists) ambao walifahamu hili pia wanakubali kuwepo kwa nguvu iliyo nje ya uwezo wa viumbe hivyo kufanya kazi zao, lakini wanayawekea mpaka maelezo yao kuhusu mada hii kwa kuiita nguvu hii “silika.” Kwa kuwa hawataki kumtambua mmiliki halisi wa nguvu hii wanaiita silika, vile vile wanaizulia jina na kuiita “maumbile mama.” Hata hivyo, hadi sasa, hakuna mfuasi wa nadharia ya mgeuko ambaye ameweza kuonyesha kuwa hicho wanachokiita silika kinapata amri na maelekezo kutoka wapi, kukielezea kile wanachokiita “maumbile mama”, kueleza iwapo kama ni jiwe, mti, mto, mlima, bahari au nyota.

Matokeo yake, wafuasi wa nadharia hiyo wamemtengeneza mungu wa kufikirika kutokana na kile wanachokiita “maumbile mama” na kutumia neno “silika” kwenye tabia inayotokana na amri na maongozo ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anasema ndani ya Qur’an Tukufu:

“Hamuabudu badala yake ila majina tu mliyo yapanga nyinyi na baba zenu. Mwenyezi Mungu hakuyateremshia hayo uthibitisho wowote…” (Qur’an 12: 40)

Hivyo, kwa kuukataa ukweli wa mambo, wanajidanganya na kujaribu kuzifurahisha na kuzituliza dhamiri zao. Wanahisi kwa uwazi kabisa uwepo wa Mungu na sifa zake katika dhamiri zao, lakini wanaukimbia  “ukweli” na kuukana ushuhuda wa Mwenyezi Mungu. Sababu ya suala hili imeelezwa ndani ya Qur’an kama ifuatavyo:

“Basi zilipo wafikia Ishara zetu hizo zenye kuonyesha, wakasema: Huu ni uchawi dhaahiri. Na wakazikataa kwa dhulma na kujivuna, na hali ya kuwa nafsi zao zina yakini nazo. Basi angalia ulikuwaje mwisho wa mafisadi!” (Qur’an, 27: 13-14)

Mwenyezi Mungu Mtukufu umeutandaza ushahidi wa uwepo Wake mbele ya macho ya mwanadamu. Akaufanya ujuzi Wake wa milele ujidhihirishe ndani ya viumbe wake wateule. Kwa fadhila zake zisizokuwa na kikomo, amewapa kazi kubwa viumbe wasiotarajiwa, dhaifu kabisa na hata wasiokuwa na ubongo. Matokeo yake, viumbe wengi, wakubwa kwa wadogo, kuanzia ndege mpaka nyoka, nyangumi mpaka wadudu, huonyesha tabia na matendo yasiyotarajiwa ambayo hujaza mshangao watu wengi. Tabia na mienendo hiyo huwastaajabisha mno watu wengi. Hata mwanadamu, ambaye anajiona kuwa kiumbe mwenye akili, ujuzi na utambuzi, amekuwa dhalili mbele ya ujuzi na ustadi mwingi wa viumbe hawa ( kwa mfano, uwezo wa buibui wa kuzalisha nyuzi imara zaidi ya chuma), na hana hata uwezo wa kumuiga.

Maudhui ya mada yangu hii,yaani mbu, ni mojawapo tu ya viumbe hao, ambaye vipengele vya tabia na mwenendo wake utatujaza mshangao. Na ingawa yeye ni kiumbe ambaye tumezoea kumuona na kukutana naye sana, yumkini ni kiumbe ambaye hatumfikirii na humuona kuwa asiyekuwa na maana yoyote.

Hivyo, waweza kujiuliza, “Kama ni hivyo, kwa nini azungumziwe mbu?” Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema ndani ya Qur’an Tukufu:

“Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya kutoa mfano hata wa mbu na ulio wa zaidi yake. Ama wale walio amini hujua ya kwamba hiyo ni haki iliyo toka kwa Mola wao Mlezi, lakini wale walio kufuru husema: Ni nini analo kusudia Mwenyezi Mungu kwa mfano huu? Kwa mfano huu huwapoteza wengi na huwaongoa wengi; lakini hawapotezi ila wale wapotovu.” (Qur’an, 2: 26)

Yampasa mwanadamu anayeutambua ukweli huu autafakari kwa dhati ushuhuda wa uumbaji wa Mwenyezi Mungu na amuogope na kumkhofu Yeye tu.

“…Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu? Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ana ufalme wa mbingu na ardhi? Nanyi hamna mlinzi wala msaidizi isipo kuwa Mwenyezi Mungu.” (Qur’an, 2: 106 – 107)

 

UVIMBE KATIKA MLANGO WA KIZAZI (CERVICITIS POLYPS)

10 Feb
Uvimbe huota ndani ya kizazi (leiomyoma au Fibroid – vinyama ambavyo vipo kama uvimbe laini).
 
CHANZO NI NINI?
 
Uvimbe (fibroid au Uterine Myoma) husababishwa na kuwepo kiwango kikubwa cha mafuta katika maeneo ya kizazi na kuwepo kwa kiwango kikubwa cha Estrogen hormones.Vinyama hivi vinapokuwa katika mlango wa kizazi mwanamke huhisi kama kuna kitu ukeni kimechomoza na anapojisafisha hukigusa na anaposhiriki tendo la ndoa huhisi kuna kitu kinaguswa au kusukumwa ndani ukeni. Kinyama hicho kinapoguswa mara kwa mara husababisha mwanamke kutokwa na damu ukeni pia husababisha damu ya hedhi kutoka kiasi kidogokidogo ikiambatana na maumivu ya tumbo chini ya kitovu, kutokwa na majimaji yenye rangi ya brown ukeni yakiambatana na harufu mbaya. Tatizo hili likikaa muda mrefu husababisha mlango wa uke (cervix) hivyo hata upatikanaji wa mimba huwa na matatizo, damu ya hedhi kutoka kwa shida ikiandamana na maumivu makali ya tumbo chini ya kitovu na kutokwa na mabonge meusi ya damu’D.U.B’.
 
VIPIMO
Ultrasound,Cervical Xray na vingine kuangalia ukeni kama ambavyo Dkt. ataona vinafaa.
 
TIBA NA USHAURI
 
Baada ya uchunguzi wa kina tiba hutolewa kutokana na ukubwa au udogo wa tatizo. Ukiona dalili mathalan kutokwa na damu wakati wa tendo wahi kwa Dkt.
 
MAKALA HII IMEANDALIWA NA DOKTA ABDULAZIZI MALIKI (0714 909563/ 0763 986499)

MAMBO 10 YANAYOKUFANYA UWE MUME BORA

24 Jan
 1. Vaa vizuri kwa ajili ya mkeo, uonekane nadhifu na mwenye kunukia vizuri. Kama ambavyo mume anapenda mke wake aonekane maridadi kwa ajili yake, naye pia anapenda mume wake avae vizuri kwa ajili yake. Kumbuka kwamba Mtukufu Mtume (s.a.w) daima alikuwa akianza kupiga mswaki pindi anaporudi nyumbani na daima alikuwa akipenda harufu nzuri.
 2. Muite mkeo kwa majina mazuri. Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akiwaita wakeze kwa majina mazuri ambayo hata wao wenyewe walikuwa wakipenda kuyasikia. Muite mkeo kwa jina zuri analolipenda zaidi kulisikia, na epuka kutumia majina yatakayoumiza hisia zake.
 3.  Usiamiliane na mkeo kama nzi. Mara zote katika maisha yetu ya kila siku huwa hatukumbuki kuwa kuna nzi mpaka pale wanapotuudhi. Angalia, mkeo hukufanyia mambo mengi mema kwa siku nzima ambayo huwa huyaangalii, ila pale anapokufanyia kosa kidogo unamtazama. Usiishi naye kwa namna hii; yatambue mambo mema yote anayokufanyia.
 4.  Ukiona kosa kutoka kwa mkeo, jaribu kuwa mkimya na usiseme! Hivi ndivyo Mtukufu Mtume (s.a.w) alivyokuwa pale anapoona jambo lisilokuwa muafaka kutoka kwa wakeze. Ni njia ambayo ni wanaume wachache wa Kiislamu wameimudu.
 5.  Onyesha tabasamu kwa mkeo pindi unapomuona na daima zidisha kumkumbatia. Kutabasamu ni sadaqah na mkeo naye anastahili hiyo sadaka kwa namna ya kipekee. Fikiria maisha yatakavyokuwa pale mkeo anapokuona unatabasamu kwa ajili yake! Kumbuka pia zile hadith zinazosema kuwa Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akimbusu mkewe kabla ya kwenda kuswali, hata kama akiwa amefunga.
 6. Mshukuru kwa kila analokufanyia. Kisha mshukuru tena na tena! Angalia, mkeo anakuandalia chakula, anasafisha nyumba na anafanya kazi nyingine nyingi mno. Wakati mwingine hata kumpongeza hufanyi! Usiwe hivyo, mshukuru na useme: “Ahsante mke wangu!”
 7.  Muombe akuandikie mambo kumi uliyomfanyia na yakamfurahisha. Kisha mfanyie mambo hayo tena. Mara nyingi huwa ni vigumu kujua mambo yanayomfurahisha mkeo. Huna haja ya kubahatisha, muombe akwambie na kisha uyafanye hayo na mengine pia katika kipindi chote cha maisha yenu.
 8.  Usiyapuuze na kuyabeza matakwa yake. Mfariji. Wakati mwingine wanaume huyadharau maombi ya wake zao. Mtukufu Mtume (s.a.w) hakuwa hivyo.
 9.  Uwe mwenye kunyumbulika na fanya michezo na mkeo. Mtukufu Mtume (s.a.w) alikuwa akishindana na mkewe bibi Aisha katika mchezo wa kukimbia. Mara ya mwisho umemfanyia lini mkeo jambo kama hilo?
 10.  Daima kumbuka maneno ya Mtukufu Mtume (s.a.w): “Mbora wenu ni yule anayeitendea mambo bora familia yake. Nami ni mbora wenu kwa familia yangu.” Jaribu kuwa bora!

Usisahau kumuomba Mwenyezi Mungu aifanye ndoa yako kuwa bora.

SOSHOLOJIA YA QUR’AN 2 -JE MWANADAMU NI MWANAJAMII KWA ASILI?

18 Jan

بسم الله الرحمن الرحيم

Assalaam alaykum…

Ndugu zangu katika imani! katika sehemu ya kwanza ya mada hii, tuliangalia maana ya jamii na michanganuo yake. Na leo hii nawasilisha kwenu sehemu ya pili ya mada hii katika kuangalia iwapo mwanadamu ni mwanajamii kwa asili au la.

Hoja inayohusu mambo yanayohusika au yaliyosababisha kuibuka kwa maisha ya kijamii kwa binadamu, imekuwa ikiibuliwa kutoka nyakati za zamani. Je mwanadamu amezaliwa na silika ya kupenda kushirikiana na wengine (gregariousness)? Yaani, je kwa asili aliumbwa kama sehemu ya kitu kikubwa (ujumla), akiwa na wito ndani ya maumbile yake unaomtaka kuungana na kitu hicho kikubwa (ujumla)? Au hakuumbwa kuwa kiumbe anayependa kushirikiana na wengine (gregarious), lakini nugvu na utambuzi wa nje vikamlazimisha kuishi maisha ya pamoja? Kwa maneno mengine, je yeye kwa asili ana mwelekeo au silika ya kuishi kwa uhuru, na kwamba ana mwelekeo wa kutokubali aina yoyote ya wajibu na mipaka ambayo amewekewa, japokuwa mipaka hiyo inaweza kuwa muhimu kwa maisha ya kijamii? Je, kweli amejifunza kutokana na uzoefu kwamba hakuna mtu anayeweza kuishi peke yake, na hivyo akalazimika kusalimu amri mbele ya mipaka iliyowekwa na maisha ya kijamii? Au, ingawa yeye si kiumbe anayependa kushirikiana na wenzake (gregarious) kwa asili, sababu iliyomshawishi kukubali maisha ya kijamii haikuwa ya lazima, au angalau ulazima huo sio sababu pekee? Au, ni kwa hukmu ya akili yake na kwa kufanya ukokotozi ndiyo akafikia uamuzi wa kwamba ni kwa ushirikiano na maisha ya pamoja ndipo anapoweza kufurahia zawadi ya kuumbwa kwake na hivyo akachagua kuishi katika ushirikiano na wanadamu wengine? Kutokana na hali hii, hoja hiyo inaweza kuwekwa katika njia tatu:

1.Je mwanadamu ni mwanajamii kwa asili?

2.Je mwanadamu ni mwanajamii kwa kulazimishwa?

3.Je mwanadamu ni mwanajamii kwa hiari yake na uchaguzi wake mwenyewe?

Kwa mujibu wa nadharia ya kwanza, maisha ya kijamii ya mwanadamu ni sawa na ushirikiano wa mwanaume na mwanamke katika maisha ya ndoa; kila mmoja wa washirika ameumbwa kama sehemu ya kitu kizima, na, kwa asili, anatamani na anataka sana kuungana na kitu hicho kizima. Kwa mujibu wa nadharia ya pili, maisha ya kijamii ni kama ushirikiano, kama vile mkataba kati ya nchi mbili ambazo zikiwa moja moja haziwezi kujitetea dhidi ya adui anayewakabili wote, na jambo hilo linawalazimisha kufanya makubaliano ya kushirikiana. Kwa mujibu wa nadharia ya tatu, maisha ya kijamii ni sawa na ushirikiano wa mabepari wawili, ambao huibua usuhuba wa kibiashara, kilimo au uzalishaji unaolenga kupata faida kubwa.

Kwa msingi wa nadharia ya kwanza, sababu kuu ya mwanadamu kuwa katika maisha ya kijamii ni ya asili ambayo imo katika maumbile na silika yenyewe ya mwanadamu. Kwa msingi wa nadharia ya pili, sababu kuu ni kitu kingine kabisa kutoka nje ya asili na silika ya mwanadamu na ambacho hakitegemei silika hiyo. Na kwa mujibuwa wa nadharia ya tatu, sababu kuu inayohusika na maisha ya kijamii ni akili na na kipawa cha mwanadamu mwenyewe.

Kulingana na maoni ya kwanza, udamisi/uanajamii (sociability) ni lengo kuu na la wote ambalo kwa asili mwanadamu anataka, anatamani na anagombania kulifikia. Kwa mujibu wa nadharia ya pili, udamisi/uanajamii (sociability) ni jambo la kawaida na limetokea tu kama ajali, ni jambo la pili na la ziada na sio lengo la awali na la msingi. Kwa mujibu wa nadharia ya tatu, udamisi/uanajamii (sociability) ni matokeo ya akili na uwezo wa mtu wa kuhoji na kudadisi.

Baada ya kuziangalia hizo nadharia tatu kuhusu uanajamii wa mwanadamu, ni upi msimamo wa Qur’an Tukufu katika hizo nadharia? Je ni nadharia ya kwanza, ya pili au ya tatu? Ili kuyajibu maswali haya, basi ungana nami katika sehemu ifuatayo ya mada hii.

Nakutakia siku njema…

Kwa maoni: 0712 566595/0772 403100/ 0763 348213/0685 590949